Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania,IGP Simon Sirro akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Msumbiji,IGP Bernardino Rafael baada ya kuwasili mkoani Mtwara kwa ajili ya kikao cha pamoja.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanyika kwa mazungumzo, IGP Sirro alisema kimsingi kikao hicho kilikuwa cha kazi na wamekubaliana mambo ya kufanya kwa lengo la kupambana na wahalifu wachache wanaotaka kuchafua heshima na amani ya nchi hizo lazima washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

“Tumekubaliana kimsingi kwamba wahalifu siku zote hawana mipaka kwa hiyo na sisi mipaka isitufanye tukashindwa kupambana na uhalifu na hasa haya makosa yanayovuka mipaka ni lazima tushirikiane na kikubwa zaidi ni kubadilishana taarifa na kufanya operesheni za pamoja,” alisema IGP Sirro

 

“Na mambo mengi tumekubaliana hao wahalifu wachache wanaotusumbua ikiwemo na wale waliofanya mauaji ya Watanzania na watu wa Msumbiji kuhakikisha tunawakamata na sheria kuchukua mkondo wake. Kimsingi tumekubaliana mambo ya kufanya ambayo mwisho wa siku yatakuwa majibu mazuri kwa Tanzania na Msumbiji,” alisema IGP Sirro

Alisema wananchi hawana sababu ya kuwa na wasiwasi na kwamba yeye na mwenzake wa Msumbiji wameshawaelekeza kamanda wa polisi wa eneo la Msumbiji na kamanda wa Mtwara kwenda kuzungumza na wananchi na kisha kwenda eneo la tukio kuona upelelezi na matukio yaliyotokea na baada ya hapo Watanzania waliokwenda Msumbiji kulima watachukua mali zao na kurudi nchini.

Naye IGP wa Msumbiji, Rafael aliomba Jeshi la Tanzania vinapotokea vitendo viovu kama ilivyotokea mauaji waweze kufika eneo la tukio kutoa msaada kutokana na umbali uliopo nchini mwao hadi kufika ulipo mpaka wa nchi hizo.

Related Posts