WATAKIWA KUFICHUA WANAOFANYA VITENDO VYA UKATILI.

Na A/INSP Frank Lukwaro

Wananchi wametakiwa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya ukatili wa Kijinsia hususani kwa Wanawake na Watoto ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikiathiri  ukuaji wa uchumi kwa jamii kubwa hapa nchini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwaza Mhandisi Robert Gabriel wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia zilizoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto katika Viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza.

Amesema Ukatili wa Kijinsia ni kikwazo cha maendeleo katika Nyanja za Kiuchumi, kisiasa na maendeleo hivyo kila mmoja anapaswa kuhakikisha kuwa anafanya wajibu wake kwa kutoa taarifa mapema katika Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi pamoja na mamlaka nyingine ili kuhakikisha kuwa unyanyasaji unakomeshwa.

Amesema vitendo hivyo hivyo vinarudisha nyuma ajenda ya kuleta maendeleo hapa nchini kwa kuwa muda mwingi unatumika katika kutatua migogoro na kesi za ukatili ambapo  muda huo ungeweza kutumika vyema katika kuwaletea maendeleo Wananchi na wao wenyewe kujikita katika shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Jinsia na Watoto Kutoka Makao Makuu ya Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Faidha Suleiman amesema wameamua kufanyia maadhimisho hayo mkoani Mwanza kwakuwa baadhi ya Wilaya za mkoa wa Mwanza zimeonekana katika takwimu kuonesha kuwa bado kuna tatizo kubwa la mimba za utotoni ambao pia ni ukatili.

Amesema katika Maadhimisho hayo watajikita kutoa elimu kuhusu Dawati hilo na hatua za kufuatwa pindi wananchi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili pamoja na kutoa misaada katika Shule zinazolea watoto wenye mahitaji maalumu.

Aidha ,amesema wakiwa katika mkoa huo wameweza kutembelea Shule ya Msingi Mitindo iliyopo Wilayani Misungwi ambayo inatoa huduma kwa watoto wenye mahitaji maalumu ambapo wamewapatia mahitaji mbalimbali ambayo yatawasaidia katika masomo yao.

Naye Afisa Mwandamizi wa Shirika la Kivulini Mwanza Bi. Grace Mussa amesema wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa elimu jambo ambalo limeongeza uelewa wa vitendo vya ukatili kutokana na kuongezeka kwa taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika vituo vya Polisi.

Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi yalishirikisha wadau mbalimbali Vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Asasi za Kirai, Wanafunzi wa Vyuo, Sekondari na Msingi pamoja na Watendaji wote wa Dawati la JInsia na Watoto kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akizungumza katika Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia zilizoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto na kufanyika katika Viwanja vya Nyamagana Mwanza ambapo maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa ukatili wa kijinsia pamoja na Watendaji wa Dawati kutoka Tanzania bara na Zanzibar.(Picha na A/INSP Frank Lukwaro wa Jeshi la Polisi)

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ya Polisi Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Faidha Suleiman wakati wa Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia zilizoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto na kufanyika katika Viwanja vya Nyamagana Mwanza ambapo maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa ukatili wa kijinsia pamoja na Watendaji wa Dawati kutoka Tanzania bara na Zanzibar.(Picha na A/INSP Frank Lukwaro wa Jeshi la Polisi)

Baadhi ya Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka mikoa mbalimbali wakiwa katika maandamano wakati wa Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia zilizoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto na kufanyika katika Viwanja vya Nyamagana Mwanza..(Picha na A/INSP Frank Lukwaro wa Jeshi la Polisi)

Wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Mitindo ya Wilayani Misungwi wakiimba wakati wa Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia zilizoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto na kufanyika katika Viwanja vya Nyamagana Mwanza..(Picha na A/INSP Frank Lukwaro wa Jeshi la Polisi)

Related Posts