Jela miaka 5 kwa kosa la kujipatia fedha na mali kwa njia ya udanganyifu.

Na: Jeshi la Polisi

Mahakama ya Wilaya Wete katika Mkoa wa Kaskazini Pemba imemuhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitano mshitakiwa Said Mohammed Amour baada ya kupatikana na hatia kwa makosa mawili ikiwemo  la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na jengine la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Akisoma hukumu hiyo hakimu wa mahakama hiyo Salim Talib alusema kuwa “Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Mahakama imemkuta mtuhumiwa na makosa hivyo inamuamuru kutumikie kifungo cha miaka 5 na pia imemuamuru mshitakiwa kurudisha mali na fedha hizo kwa mlalamikaji kwa kadri itakavyowezekana”.

Kwa upande wake mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Zanzibar Juma Mussa Omar kabla ya kusomwa hukumu hiyo ameiomba Mahakama itoe adhabu kali na stahiki kwa mshitakiwa kama ilivyoelezwa kwenye sheria ili mshitakiwa apate kujifunza na kujionya kutokana na kitendo cha aina hiyo pamoja na jamii Kwa ujumla.

Kabla ya kusomwa hukumu hiyo mshitakiwa alipata fursa ya kujitetea ambapo aliiomba Mahakama hiyo impunguzie adhabu na ikiwezekana imtoze faini ombi ambalo limekataliwa na mahakama hiyo.

Katika kesi hiyo ilidaiwa kwamba mwezi Oktoba mwaka 2020 huko Kipangani Wilaya ya Wete,Mkoa wa Kaskazini Pemba bila ya halali na kwa njia ya udanganyifu mshitakiwa alijipatia bangili 4, pete 3, herini pea 2, mkufu 1, lakti 2, vyote vikiwa vya madini ya dhahabu pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi 9,000,000/ vyote vikiwa na thamani ya shilingi 17,850,000/ kutoka kwa Bi Safia Ali Said baada ya kumwambia ampatie mali na fedha hizo kwa ajili ya kufanyiwa dawa wakati hakua na dhamira ya kufanya hivyo jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kosa hilo ni kinyume na k/f 299 cha  kanuni ya adhabu namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kesi hiyo yenye kumbu kumbu Wete DM 26 ya mwaka 2021 kwa mara ya kwanza ilianza kusikilizwa Mei25, mwaka jana na Jumla ya mashahidi 8 walifika na kutoa ushahidi wao mahakamani hapo.

Related Posts