Na. Jeshi la Polisi – Dodoma.
Jeshi la Polisi Makao Makuu Dodoma, Kamisheni ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai wamepokea kompyuta 10 kutoka Kampuni ya Suoerdoll kwa ajili ya kusaidia shughuli za Upelelezi wa Makosa ya Jinai hapa Nchini.
Kompyuta hizo ni pamoja na kumpyuta mpakato 5 aina ya HP Pavilion Core i7, Printa moja aina ya Laser Jet MFP 454 DW.
Akipokea msaada huo Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini DCI Camilius Wambura amesema vifaa hivyo vya kisasa ni msaada muhimu kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa vitasaidia katika ufanyaji kazi wa Jeshi ikiwemo kutunza kumbukumbu na kuchakata taarifa mbalimbali za uhalifu sambamba na kuendana na kasi ya maendeleo ya dunia katika kuzuia na kubaini vitendo vya kihalifu nchini.
Aidha DCI wambura amesema kuwa baadhi ya changamoto zinazoikabili Jeshi la Polisi nchini ni uchakavu na uhaba wa vitendea kazi ambapo amewaomba wadau wengine kujitokeza katika kusaidia ili kurahisisha upelelezi na uimarishaji wa Usalama wa raia na mali zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Superdoll nchini Seif Ali Seif amesema jamii inawajibika katika kulisaidia Jeshi la Polisi kwakuwa linamajukumu makubwa ya kulinda Usalama wa Raia na mali zao
“ Tunaelewa mambo mnayoyafanya ambayo yanasababisha jamii yetu kuendelea kuishi kwa amani na utulivu sambamba na kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani na kuvutia wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza nchini sambamba na kuvutia watalii hivyo hatuna budi sisi kama wadau kuendelea kusaidia kila tunapopata fursa hiyo”.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Superdoll Ibrahim Ali amesema kampuni yake imetoa vifaa vya kisasa kwa Jeshi la Polisi kwakuwa linajua na linathamini kazi zinazofanywa na Jeshi la Polisi na vifaa hivyo endapo vitatumika vizuri basi vitaleta tija kwa Jeshi la Polisi na Tanzania kwa ujumla”.