Polisi yaadhimisha siku ya mtoto wa Afrika wilayani simanjiro mkoa wa Manyara.

Na. A/INSP Frank Lukwaro- Jeshi la Polisi

Jamii imetakiwa kufichua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto katika jamii ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema kwa lengo la kuwalinda watoto dhidi ya vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikiongezeka katika siku za hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Dkt Suleiman Serera wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto na kushirikisha Wadau mbalimbali nakufanyika katika viwanja vya Mwenge ambapo pia yamehudhuriwa na Watendaji wa Dawati hilo kutoka Mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar

Kwa Upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ya Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Maria Nzuki amesema lengo la kufanya maadhimisho hayo ni kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kupunguza na kutokomeza vitendo hivyo na pale vinapotokea hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Benjamin Kuzaga alisema wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vinakomeshwa katika Mkoa wa Manyara.

Naye Mwakilishi Shirika la SOS Children Village Bw.Mpeli Kalonge  akizungumza katika maadhimisho hayo amesema wataendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ikiwemo Dawati la Jinsia na Watoto ili kuhakikisha kuwa Watoto wanakuwa Salama dhidi ya Vitendo vya Kikatili.

Maadhimisho hayo yalitanguliwa na maandamano yaliyobeba jumbe mbalimbali yalianzia Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Simanjiro hadi Uwanja wa Mwenge na kuwashirikisha wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi katika Wilaya ya Simanjiro.

Related Posts