• "NIDHAMU HAKI WELEDI NA UADILIFU, MSINGI WA MAFANIKIO YETU"
Close

Siri ya mafanikio mambo ya ndani kuibuka mshindi wa kwanza michezo ya mei mosi 2023

Wizara ya Mambo ya  Ndani ya Nchi imeibuka kidedea  kwa kuwa mshindi wa kwanza kwa matokeo ya jumla kwenye mashindano ya michezo ya kusherehekea sikukuu ya wafanyakazi dunia (Mei Mosi) ambayo kitaifa yalifanyika mkoa wa Morogoro.

Timu zilizoshiriki mashindano hayo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ziliundwa na wachezaji kutoka idara mbalimbali zilizoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulishoo vya Taifa (NIDA) pamoja na Jeshi la Zimamoto.

Timu hiyo ya Wizara ya Mambo ya Ndani iliyoundwa na idara zake zimecheza na Wizara mbalimbali zikiwemo Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ikulu, Tanesco, TPDC, TRA, TANAPA pamoja na Benki ya  CRDB lengo likiwa ni kuimarisha afya za wafanyakazi na kujenga mahusiano na ushirikiano kati ya taasisi zilizoshiriki.

Katika mashindano hayo michezo iliyochezwa ni riadha, kuvuta kamba, mpira wa pete, mpira wa wavu, mpira wa miguu, mbio za baiskeli, mchezo wa bao pamoja na mchezo wa karata.

Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa mshindi wa kwanza kwa matokeo ya jumla baada kufanikiwa kuwa mshindi wa kwanza katika mchezo wa bao, mshindi wa kwanza katika mchezo wa baiskeli, mshindi wa kwanza riadha, mshindi wa kwanza mpira wa miguu, mshindi wa kwanza mchezo wa wavu, mshindi wa pili mchezo wa kuvuta kamba pamoja na kuwa mshindi wa pili katika mchezo wa karata jambo lililopelekea  kuibuka kuwa mshindi wa jumla katika mashindano hayo.

Katika kusherehekea ushindi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya aliwapongeza Manahodha wa timu za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na wachezaji wote walioshiriki michezo hiyo kwa kushiriki vyema michezo na kufanikiwa kuleta ushindi uliowafanya kuibuka mshindi wa kwanza katika mashindano hayo.

Aidha katika kuwapongeza wanamichezo hao, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kaspar Mmuya pia alishiriki katika hafla ya kukata keki maalumu iliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani iliyofanyika katika ukumbi wa Bwalo la JKT Umwema ikiwa ni kujipongeza kutokana na ushindi huo baada ya kutamatika kwa Mashindano ya Mei Mosi.

Vilevile, Mhe. Kaspar Mmuya aliwataka wanamichezo hao kuendeleza hamasa hiyo katika suala la kupambana na vitendo vya kihalifu vinavyotokea katika jamii, kwa kuhamasisha vijana kushiriki katika michezo ili kujenga afya na kuibua vipaji badala ya kujihusisha katika makundi ya kihalifu na vitendo vya kihalifu.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Michezo Makao Makuu ya Polisi Dodoma ACP Jonas Mahanga,  alisema kuwa Wanamichezo wa timu zote za Wizara ya Mambo ya Ndani wanaume kwa wanawake siri kubwa iliyowawezesha kuibuka na ushindi wa vikombe na medali katika michezo waliyoshiriki ni kutokana na kuwa na bidii katika kufanya mazoezi, kuonesha nidhamu wakati wote wa michezo, wachezaji kuwa na morali na utayari wa kujifunza pamoja na kunolewa vizuri na Kocha wa timu hiyo.

Naye SGT Ramadhani Nassoro ambaye alikuwa kocha wa timu ya mpira wa miguu na aliyeiwezesha timu hiyo kuibuka mabingwa wa mashindano hayo alisema kuwa Ushindi huo umechangiwa na ushirikiano thabiti uliokuwepo miongoni mwa wachezaji, taasisi walikotoka na Wizara.

Related Posts