Jeshi la Polisi nchini linatarajia kushiriki Michezo ya Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa Nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO Games) kuanzia Machi 21 hadi 27 nchini Rwanda.
Akiwaaga Wanamichezo hao na kuwakabidhi bendera ya taifa kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi leo Makao Makuu ya Polisi Jijini Dodoma, Kamishna wa Intelejensia ya Jinai Charles Mkumbo amewataka kuhakikisha wanarejea na ushindi ili kuiletea sifa Tanzania na Jeshi la Polisi.
Kamishna Mkumbo alisema Jeshi hilo lina sifa kubwa katika Michezo hivyo kila mmoja aliyepata nafasi ya kuwakilisha ahakikise anafanya vizuri na kurejea na medali ili lengo lake la kwenda liweze kutimia.
Aidha alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura kwa kuruhusu wanamichezo hao kushiriki jambo ambalo linatekeleza adhma ya Mhe Rais Samia Suuhu Hassan katika kukuza michezo nchini.
Naye Kamishna wa Polisi Jamii Faustine Shilogile amesema Wanamichezo hao wapo tayari kuliwakilisha taifa na wamefanyiwa mchujo na waliochaguliwa wote wana vigezo vya kimataifa.
Wanamichezo walioondoka leo ni 82 na wanatarajia kushiriki michezo saba ambayo ni Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu, Riadha, Vishale, Judo, TAEKWONDO na Shabaha.